Fumanizi lililotokea Kinondoni.
...Hili Makumbusho.
Haruni Sanchawa na Makongoro Oging'
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Sophia Simba
amekuja juu akisema mmomonyoko wa maadili katika jamii ndiyo
unaochangia kwa sehemu wana ndoa kufumaniana kila kukicha.
Akizungumza na gazeti hili, juzikati jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa
Simba alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, viongozi wa dini nao
wanahusika sana kwani wakiwa kwenye mimbari zao hawaneni na waumini wao
kuhusu dhambi hiyo kuu ya usaliti.
“Kwanza vitendo vya kufumaniana
vinaathiri watu kisaikolojia na kuharibu uhusiano kati ya mke na mume,
hivyo kusumbua watoto endapo wana ndoa hao watakuwa wamefanikiwa kuwa
nao,” alisema.
Fumanizi la Buguruni.
Katika mahojiano hayo, Waziri Simba alisisitiza kuwa tatizo la wana
ndoa kufumaniana ni kubwa na sasa linazidi kuota mizizizi kutokana na
watu kutozingatia maadili ya Kitanzania na yao wenyewe.
“Katika
hili, serikali haiwezi kukomesha tatizo, bali taasisi husika, mashirika
mbalimbali yanayojishughulisha na masuala ya maadili wakiwemo viongozi
wa dini, wote washirikiane kwa pamoja ili kuweza kutoa elimu ya kiroho
kwa wananchi na kuwaambia madhara ya dhambi hiyo,” alisema.
Pia waziri huyo aliitetea serikali iliyopo madarakani akitaka isibebeshwe mzigo wa lawama kuhusu hilo.
“Kuna mambo ambayo serikali inaweza kufanya yenyewe na mengine lazima
kushirikisha taasisi zingine kwa hiyo katika hili serikali isibebeshwe
mzigo wa lawama hata kidogo.”
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Sophia Simba.
Aliongeza kuwa suala la mapenzi kufanywa hovyohovyo ni hatari na
ndiyo maana mtu anapofikia umri wa kuoa au kuolewa hufanya hivyo kwa
lengo la kujenga familia badala ya kuzunguzunguka.
Uchunguzi
uliofanywa na timu ya waandishi wetu umebaini kuwa wana ndoa ndiyo
wanaongoza kwa kufumaniana kuliko wachumba au wapenzi japo imani
hazikubaliani na makundi hayo kukutana kimwili kabla ya ndoa.
Katika
Jiji la Dar es Salaam peke yake, inakadiriwa kuwa kila baada ya siku
mbili kunatokea fumanizi kwenye vitongoji vyake huku wanaume wakiongoza
kwa kufumaniwa wakiwa na wanawake wengine.
Utafiti zaidi umegundua
kuwa, mafumanizi mengi ya miaka ya karibuni yanachangiwa na simu za
mkononi, hasa watu kupanga usaliti kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu
‘SMS’.
Aidha, kesi nyingi zinazofikishwa polisi zikihusu fumanizi
huishia kwa wagoni kuelewana au kulipana fidia lakini wanawake ndiyo
wanaathirika zaidi kwani wengi wanaofumaniwa huachika.