Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akizungumza waandishi wa
gazeti la Mwananchi katika mahojiano maalumu ofisini kwake Makao Makuu
ya chama hicho, jijini Dar es Salaam wiki iliyopita. Picha na Edwin
Mjwahuzi
“Kushushwa juu ya fuso na mabomu kwenye kebini umebaki peke yako watu
wote wamekimbia. Ndiyo wamekimbia...nimebaki na mlinzi wangu tu pale juu
ya gari. Polisi walipoona vile walinifuata na kunirushia mabomu ya
machozi na kunifanya nishindwe kupumua kwa dakika tano mfululizo.”
Hii ni sehemu ya ushuhuda wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuhusu misukosuko ya maisha yake kisiasa.
Ni sehemu ndogo iliyojaa taswira ya ukatili, lakini pia nguvu ya ushindi katika harakati za kawaida za kuleta mapinduzi.
Kwa wengi wanaomfahamu Dk Slaa na mambo ambayo hukumbana nayo huenda
wasiupe uzito ushuhuda huo, lakini kwa kiongozi huyo machachari
aliyegombea urais mwaka 2010 na kushindwa na Rais Jakaya Kikwete wa CCM,
hilo ndiyo tukio ambalo anasema hatalisahau katika maisha yake yote kwa
sasa.
“Baadaye nikamwambia mlinzi wangu hebu tuteremke huku juu...na polisi
walipoona vile wakatufuata tena na kuendelea kutumiminia risasi, nikaona
watatuua. Vijana wangu walipoona vile wakaniambia Dokta ruka!
”Sasa narukaje kutoka kwenye kebini hadi chini? hapa mimi nikawaeleza
nitateremka vipi wakaniambia mzee serereka...bahati nzuri nikaserereka
na ule mlango na nilipofika nusu wakaniambia ruka.
“Nilipofika katikati nikaruka, kumbe chini ya gari kulikuwa na vijana
wawili nao wamejificha pamoja na mlinzi wangu, tukawa wanne.”
Hii ni simulizi ya Dk Slaa wakati akijibu swali aliloulizwa katika
mahojiano maalumu na gazeti hili wiki iliyopita kuhusu ni jambo gani la
kusikitisha ambalo hatolisahau kwa umri wake hasa tangu alipotoka
upande wa pili (upadri) kuingia katika siasa.
Anajibu kuwa ilikuwa ni mkutano uliofanyika Novemba 8 kuamkia Novemba 9
mwaka 2011 ambao ulifanyika Arusha wakati Mbunge wa Jimbo hilo, Godbless
Lema alipovutana na polisi kuhusu kutoka kwake mahabusu na siku hiyo
ilikuwa Lema aachiwe na wananchi walijitokeza kwa wingi mahakamani
kusubiri kuachiwa kwake.
Baada ya kuona umati huo polisi wakapeleleza nani anaweza kuondoa umati
huu, wakaambiana, Dk Slaa au Mbowe (Freeman Mbowe- Mwenyekiti wa
Chadema aliyekuwa Arusha), wakaona wanipigie simu na mimi nilikuwa chuo
kimoja kilichoko Usa River Arusha natoa mada. Nikawaeleza siwezi kuja,
wakaniuliza hadi saa ngapi nikawaeleza hadi saa tisa wakakubali
wakaniambia tutakusubiri dokta.
Wananchi walikuwa wengi siku hiyo baada ya kusikia kwamba Lema
ataachiwa. Nilipofika nilikuta umati mkubwa sana wa watu hadi nikaogopa
kwa kuwa sikuwa hata na vipaza sauti, hivyo nikajiuliza nitawahutubiaje
wananchi hawa na wanisikie?
Siku hiyo baada ya mvutano wa Lema na polisi hawakuwa wamemleta
mahakamani na wananchi walijua yupo wamemfungia, jambo lililozua vurugu
lakini nilipofika polisi wakanieleza tuwapeleke wapi wao wakasema
tuwapeleke uwanjani.
Mimi, nikawaeleza mleteni Lema hata kama bado mnataka kumshikilia na
tukimaliza mtamchukua ili tutulize munkari wa wananchi hawa, mwanzo
walikubali, lakini baadaye walikataa na ilipofika saa 11 jioni wakasema
hawatamleta hadi kesho yake saa 12.00 asubuhi.
Nikakubali, tukakesha uwanjani hapo wakati mvua kubwa inanyesha, lakini
tulipata taarifa kwamba polisi wanajiandaa kutupiga mabomu. Mimi
nikawaeleza haiwezekani kwa kuwa wao ndiyo wametuambia tukae hapa,
lakini ilipofika saa 11 alfajiri tuliona mabomu yakimiminika watu
walikimbia na kubaki mimi na mlinzi wangu.
Baada ya kuteremka nilipanda ndani ya gari na mlinzi wangu nikafunga
mlango kwa kutumia bolt, lakini tulivyopandisha kioo kikagoma ikabidi
tukae hivyo hivyo hadi saa 12.30
Chini tunawasikia polisi wakisema mshenzi huyu nimempiga risasi tatu za
moto, lakini yuko wapi walijua watakuta maiti chini ya gari.
Ilipofika saa 12.30, mimi nikawaambia tushuke chini kwa kuwa watalivuta
gari hili hadi kituo cha polisi na watatukamata. Nikafungua mlango na
nikawaita askari na kuwaambia polisi wangu mpooooo..... mmoja akaweka
sawa silaha yake, lakini kwa kuwa mkuu wake alikuwapo akawazuia. Hakika
tukio hili sitolisahau.
Swali: Kuna malalamiko kuwa
ruzuku ambayo chama chenu kinapata huwa haifiki katika ngazi ya chini ya
chama. Matumizi ya ruzuku hii ni yapi?
Dk Slaa: Tuliamua kubadili matumizi ya ruzuku hii ambayo tunaipata
kutoka serikalini, Sh233 milioni kila mwezi kwa kununua vitendea kazi na
kuvipeleka katika majimbo na kanda zetu zilizopo nchi nzima lengo ni
kujenga chama kuanzia ngazi ya chini.
Tuliamua kuchukua uamuzi huo baada ya fedha tulizokuwa tukizipeleka kila
mwezi kugombaniwa na viongozi, matokeo yake hazifanyi kazi kama
tulivyokusudia.
Leo hii Chadema ina kanda kumi ambazo zote tumezinunulia gari moja na
upande wa majimbo nayo tumenunua pikipiki moja nchi nzima, hivyo hayo
ndiyo matumizi ya ruzuku.
Kanda na majimbo yanajiendesha kwa kutumia kadi zaidi ya milioni 75
ambazo tumezipeleka nchi nzima, kila kadi ni Sh1500 na ada ni Sh1000,
lakini kuna maeneo kadi hii inauzwa kwa Sh10,000 na nilikwenda Mwanza
hivi karibuni nikakuta kiongozi wangu kaweka rehani kadi ili akopeshwe
fedha. Hii inaonyesha ni jinsi gani kadi hizi zilivyo na thamani.
Swali: Chadema ni moja ya
vyama vinavyojipambanua kupambana na ufisadi nchini. Hata hivyo, taarifa
zilizopo zinaonyesha kuwa hakijatoa ushirikiano wa mahesabu yake
kukaguliwa na CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali). Nini
maoni yako juu ya jambo hili?
Dk Slaa: Serikali kwa kukurupuka ilitengeneza sheria na haikutengeneza
kanuni. Sisi Chadema tangu mwaka 2007 tunakaguliwa na wakaguzi wa ndani
wanaoidhinishwa na Kamati Kuu na Baraza Kuu la Chadema. Baada ya kuona
hili mimi nilikwenda ofisi ya Msajili wa Vyama kuuliza kanuni ipo wapi,
mpaka leo hii sijajibiwa na ukweli ni kwamba hakuna kanuni ya ukaguzi
sasa unakaguliwa na unatoa ripoti katika mfumo upi?
Mwaka 2012, ofisi ya msajili ilituandikia barua kwamba vyama vya siasa
vitakaguliwa na vyama vitalipa vyenyewe. Sisi Chadema hatukukubali kwani
fedha zinazokaguliwa zimetoka serikalini na mkaguzi wangu wa ndani
anatukagua kwa Sh2 milioni, lakini akija mkaguzi tutakaguliwa kwa zaidi
ya Sh50 milioni sasa kwa gharama hii hatuiwezi.
Swali: Operesheni yenu ya M4C
imefanyika kwa muda mrefu katika mikoa mbalimbali nchini. Je, ni maeneo
gani mmegundua ni magumu kwenu kuyapenya na kujiimarisha? M4C
imekisaidia vipi chama, kiasi gani kimetumika kuifanikisha?
Dk Slaa: Ngoja niwaeleze, katika operesheni hiyo hakuna eneo ambalo
Chadema lilikuwa gumu kwake bali kila eneo lilikuwa ni rahisi na
wananchi walituelewa vizuri sana wakati wa mikutano yetu.
M4C imekifanya chama kujipambanua hadi vijijini tofauti na ilivyokuwa
mwanzo kwa CCM kutawala nchi nzima lakini leo hii kama ni mpira wa miguu
CCM ina wachezaji 11 uwanjani hivyo hivyo na Chadema ina wachezaji 11
na tutaendelea na operesheni hii hadi 2015 katika uchaguzi mkuu.
Swali: Kila uchaguzi mkuu na
uchaguzi mdogo wa ubunge kila zinapofanyika chama chenu hulalamika kuwa
kuna wizi wa kura unaofanywa na CCM. Je, Mmeshagundua wizi huo wa kura
unavyofanyika?
Dk Slaa: Afadhali nimeulizwa swali hili kwani watu wanatuona kama
Chadema ni walalamikaji tu. Unajua uchaguzi kimsingi ni uwanja wa mpira.
Tunapolalamika tunakuwa na hoja.
Mfano katika chaguzi ndogo za Kalenga, Arumeru, tulibaini vituo 20 hewa
na Igunga tulibaini daftari la kudumu la wapigakura kuwa limeboreshwa
wakati tangu uchaguzi wa mwaka 2010 tunajua kuwa daftari hili
halijafanyiwa marekebisho yoyote sasa kwa njia hii ndivyo ambavyo CCM
imekuwa inaiba na njia hiyo hiyo hadi katika uchaguzi mkuu wanavyofanya.
Swali: Baada ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2010 mlitangaza kwamba hamtashirikiana na Rais Jakaya Kikwete
kuonyesha kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais. Lakini hivi sasa
mnaonekana kushirikiana naye katika mambo mbalimbali. Je mlibadili
uamuzi wenu?
Dk Slaa: Kuna tofauti kati ya kumtambua na kufanya kazi na mtu, kuna
rais mwingine Ikulu.... kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania akishatangazwa
rais huwezi kubadili, tunafanya naye kazi kwa kuwa hakuna jinsi lakini
unaweza kuwa rais kisheria, lakini siyo kisiasa.
Tunafanya kazi na Rais (Kikwete) kwa kuwa hakuna jinsi na ndiyo maana
hata yeye anajua haendi katika mambo ya kawaida kwa wananchi hadi
unapofika wakati wa kwenda kufungua tu miradi lakini kisheria ni Rais
halali.
Swali: Utamkumbuka kwa jambo gani Rais Kikwete katika uongozi wake?
Dk Slaa: Sina la kumkumbuka Kikwete. Hakuna jambo lolote alilolifanya
litakalonifanya nimkumbuke zaidi ya kuzidisha ugumu wa maisha tu kwa
Watanzania.
Leo hii Watanzania wanalala bila kupata mlo hata mmoja, huduma za afya,
maji na elimu bado imekuwa tatizo sasa kwa hali hiyo mimi nimkumbuke kwa
lipi? Sina la kumkumbuka.
Kipindi alipoingia madarakani mwaka 2005 alikuwa na kaulimbiu ya nguvu
mpya, ari mpya na kasi mpya lakini leo hii yeye mwenyewe kaulimbiu yake
ameikimbia, sasa mimi nimsifu au nimkumbuke kwa lipi katika uongozi
wake?
Swali: Wabunge wa
NCCR-Mageuzi, David Kafulila na Felix Mkosamali walikuwa wanachama wenu,
lakini baadaye waliondoka kutokana na kutoelewana na baadhi ya
viongozi. Je, chama kinasikitika kuondoka kwao? Wakiamua kurudi
mtawapokea?
Dk Slaa: Huwezi kumzuia mtu kuchukua uamuzi wowote anaoupenda, kama Chadema hatukujuta kuondoka kwao kwani ndivyo siasa ilivyo.
Katika siasa hakuna urafiki wa kudumu na hakuna uadui wa kudumu hivyo wakiamua kurejea tutawapokea.
Swali: Ni jambo gani ambalo linakufurahisha tangu uwe Katibu Mkuu wa Chadema?
Dk Slaa: Nafurahi kuona kwamba Watanzania wa sasa siyo wale wa miaka ya
nyuma kabla ya vyama vingi vya siasa. Leo hii kila mmoja anajua haki
yake lakini pia kuidai na kuitetea yenye mwenyewe.
Hali ya Watanzania kujua haki zao haikuja hivi hivi tu kwani baadhi
wamepigwa sana, wamepoteza mali zao, wamepigwa mabomu, wamefilisika na
wengine wamepoteza maisha yao. Hivyo jambo hili kweli mimi ninafarijika
na wabunge wengi wa CCM linawaumiza sana wanaposikia maandamano.
Kiongozi yoyote wa siasa furaha yake ni pale anapoona mafanikio
yanaonekana hasa fikra na tabia kwa wananchi. Watanzania walikuwa waoga,
lakini leo wanaweza kusimama na kusema. Leo hii unaona katika
televisheni, wanawake unapofika wakati wa kudai haki za ardhi
wanavyolalamika tofauti na awali walikuwa kimya.
Swali: Imekuwa kawaida
kuwapokea wanachama wanaoachwa na CCM. Je, ikitokea wanasiasa wakongwe
wa CCM kama Frederick Sumaye au Samwel Sitta ambao wamekuwa
wakitajwatajwa kuwania urais kupitia chama hicho, ikitokea wakatoswa
huko Je, mtawapokea?
Dk Slaa: Aah....Hapo awali tulikuwa tukiwapokea kwa kuwa tulikuwa
hatujajiimarisha zaidi na tulikuwa na lengo la kujiimarisha zaidi katika
baadhi ya maeneo lakini leo hii tumekamilika kila nyanja hivyo
hatutapokea tena masalia yanayoachwa na CCM.
Swali: Mara kwa mara wabunge wenu waliopo katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wanaposhindwa kukubaliana na jambo fulani ambalo wanajua halina
masilahi kwa wanachama au taifa hutoka nje ya Bunge. Je, hatua hiyo
imekisaidia chama? Maeneo gani?
Dk Slaa: Wabunge wetu wanapotoka nje siyo kwamba wanatoka kwa kupenda
bali wanatoka kisheria lakini pia ni kupinga mabavu yanayotumika na CCM
kutokana na wingi wao.
Katika jambo hili huwezi kusema kwamba kutoka kwao kunakisaidia chama
bali kinafikisha ujumbe kwa watawala juu ya matumizi mabaya wingi wao
bungeni kuwakandamiza wananchi na sisi tutaendelea kutoka pale tunapoona
masilahi ya wananchi wanaminywa na kuporwa na wachache, tutapinga kwa
hoja na ikishindikana tutatoka.
Swali: CCM imekuwa ikidai ina mtaji wa wanachama zaidi ya milioni 5, ninyi mna wanachama wangapi?
Dk Slaa: Nina taarifa ya mkaguzi akiwataka CCM kutoa idadi ya wanachama
wao lakini hawakutoa, kama wana idadi hiyo watoe, taarifa ya CCM ya
mwaka 2010 inaonyesha walikuwa wanapata Sh9 bilioni kama ada za kadi
lakini sasa imeshuka hadi Sh2 bilioni, sasa kwa hali hiyo si idadi hiyo
imeshuka?
Sitakupa idadi kuwa Chadema tuna wanachama wangapi, kwani tuko
tunaingiza wanachama wetu katika mfumo wa teknolojia na sasa tuna ‘data
bank’ kila jimbo na kanda utakapokamilika nitawaeleza tuna wanachama
wangapi lakini uongo wa CCM hauna ukweli wowote.
Swali: Mchakato wa Katiba mpaka hapa ulipofikia ni nani wa kuunusuru?
Dk Slaa: Mwenye rungu la kutegua kitendawili hiki ni Rais Kikwete na si mtu yeyote kutoka ndani au nje ya nchi.
Rais Kikwete ndiye aliyeisaini Rasimu ya Katiba na kuipeleka bungeni
ijadiliwe na ipitishwe lakini ni yeye mwenyewe alipokwenda kulizindua
Bunge hilo akavaa kofia ya Umwenyekiti wa CCM na kuuvuruga kutokana na
kutoa misimamo yake.
Rais Kikwete achukue nafasi yake kama mkuu wa nchi. Rais wa nchi hapaswi
kuwagawa Watanzania lakini pia wakati wa mchakato wa Katiba Rais
hatakiwi kuonyesha msimamo wake hivyo achukue hatua za kuurejesha katika
reli ili uweze kuendelea.
Swali: Bunge la Katiba
linatarajiwa kuanza Agosti 5 mwaka huu na Jaji Warioba na viongozi wa
dini wamewashauri mkutane na kuondoa tofauti na CCM, pia mrejee bungeni,
haya mmeyapokeaje?
Dk Slaa: Viongozi wetu wa dini tunawapenda sana. Maaskofu wanatakiwa
kuma makini kabla ya kutoa kauli hizo kwani mwisho wa siku zitakuja
kuwahukumu.
Maaskofu wangu hawajui kilichopo bungeni, hoja yetu ni je, tunarudi
tutajadili rasimu iliyopo mezani? Hatuwezi kukubali kuona rasimu
ikichakachuliwa nasi tukakubali.
Viongozi wangu wa dini nawapenda sana ila nawasihi wasiingie katika hili
kwani litakuja kuwahukumu siku ya mwisho kwa kutoa kauli ambazo
hawajazifanyia utafiti
Swali: Baada ya Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2010 CUF waliungana na CCM na kuunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar, nanyi Chadema mliwaita CCM B lakini leo mmeshirikiana
na kuunda Ukawa Je, UCCM B unauzungumziaje?
Dk Slaa: Kama nilivyosema hapo mwanzo kwamba katika siasa hakuna urafiki
wa kudumu na hakuna uadui wa kudumu. Sisi na CUF tulitofautiana katika
malengo lakini sasa tumekaa na kuona malengo yao na yetu yanafanana
ndiyo maana tukaona tuunganishe nguvu katika jambo hili la kitaifa.
Swali: Kuna uwezekano Katiba
Mpya isipatikane mwaka 2015 mwaka ambao kutafanyika uchaguzi mkuu. Je,
kipi kifanyike ili uchaguzi huo uwe wa huru na haki?
Dk Slaa: Hata kama ikipatikana Machi au Aprili mwakani bado haiwezi
kutumika katika uchaguzi huo kwani kutakuwa na utaratibu wa kufumua
sheria zote hizo ili zifanye kazi, jambo ambalo haliwezi kutekelezeka
kwa kipindi kifupi.
Kinachotakiwa kufanyika ni kufanya marekebisho ya Katiba ya sasa ya
mwaka 1977 katika vipengele viwili vya Tume Huru ya Uchaguzi na Rais
atachaguliwa na nusu ya idadi ya wapiga kura wote.
Swali: Je, Katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 utagombea tena urais?
Dk Slaa: .....Siwezi kulizungumzia suala hili kwani kazi niliyopewa
ndani ya chama hiki kama Katibu Mkuu ni kukijenga chama kazi ambayo
nimeifanya hadi ngazi ya vijiji nchi nzima. Hivyo ukiniuliza swali hili
nitakuwa sina jibu lolote zaidi ya kukueleza kuwa kazi niliyopewa
nimeitekeleza na naendelea kuitekeleza kwa mafanikio makubwa.
Katika historia ya nchi hii hakuna kiongozi yeyote mkubwa wa chama
aliyezunguka nchi nzima, lakini wilaya zote za Tanzania nimepita kwani
nilikuwa nimebakiza wilaya ya Ngara ambayo nayo nimefika katika ziara ya
Ukawa, hivyo haya ndiyo mafanikio na jambo la urais kwangu silifikirii
kabisa.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment